TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wanamuziki ambao hutakiwi kuwakosa katika Tamasha la Sauti za Busara 2022
January 28. Tamasha la Sauti za Busara kwa miongo miwili iliyopita limekuwa na rekodi ya kuvutia ya kuonyesha vipaji vya baadhi ya wanamuziki wa Afrika katika tamasha hilo la kila mwaka ambalo limekuwa likifanyika tangu mwaka 2004.
Tamasha la mwaka huu linalokwenda na kauli mbiu isemayo “Paza Sauti: Uwezeshaji wa Sauti za Wanawake kusikika,” litafanyika Ngome Kongwe, Zanzibar kuanzia Februari 11 hadi 13.
Tamasha la mwaka huu litakuwa na zaidi ya makundi 20 ya muziki kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika yanayotarajiwa kushiriki, na wafuatao ni baadhi ya nyota wa muziki ambao sio wa kukosa kuwatazama:
Sampa The Great ni mmoja wa wanamuziki wa Afrika wa miondoko ya ‘kufoka’ (Hip Hop). Mwanamuziki huyu ana sauti inayobeba mashairi fikirishi na chokozi, yanayowavutia wasikilizaji na kuwahamisha mawazo na kuwapeleka katika dunia ya kufikirika.
Muziki wake umefungamana kutoka kughani mashairi mpaka kufoka kufoka, huku ukiwa unachochea njozi na ukiwa na hali ya huzuni ndani yake; ni muziki wa mwanamuziki kijana anayefanya kazi yake ya muziki tofauti kabisa.
Safari ya mafanikio ya Sampa imekuwa ya aina yake. Baada ya kutoa mixtape zake mbili, The Great Mixtapes (2015) and Birds na BEE9 (2017), nyota huyu mzaliwa wa Zambia na aliyekulia Bostwana alitoa album yake ya kwanza ya ‘The Return’ mwaka 2019 na kupata sifa mbalimbali duniani.
Vitali Maembe ni mwanamuziki wa Tanzania anayeheshimika nchini, mpiga gitaa, mtunzi na mwimbaji, anayefahamika kwa kupiga muziki unaofahamika ulimwenguni, lakini dhahiri akiupiga Kitanzania. Muziki wake ni muunganiko wa ladha za bara na pwani, ukichagizwa na mashairi chokozi. Akiwa anajishughulisha na muziki, Vitali Maembe lengo lake kubwa limekuwa ni kuisemea jamii, na kuwataka viongozi wala rushwa kuwajibika, pia kuibua mijadala yenye afya itakayowafanya watu kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakabili kila siku.
Msaki mara nyingi amekuwa na kipawa cha kuelezea hofu zetu za ndani, matumaini na matamanio. Yeye ni mwimbaji, mtunzi, mtayarishaji na ni moja ya talanta za kipekee na za kusisimua zinazopatikana Afrika Kusini. Ni kama yupo nyumbani katika mipangilio ya sauti pamoja na kutoa nyimbo zinazotamba katika chati za juu zaidi za muziki wa Afrika Kusini akishirikiana-kutoka Mobi Dixon hadi Revolution, Black Coffee, Black Motion, na Prince Kaybee, ambaye alifanya nao wimbo wake wa “Fetch Your Life.”
Wamwiduka Band ni kundi la muziki wa asili kutoka Mbeya, Tanzania. Kundi hilo lililoanzishwa mwaka wa 2012, linajumuisha wanamuziki wafuatao; wakiwemo Brown Isaya (mwimbaji mkuu), Adriano Wilson (mpiga gitaa kiongozi na mpiga banjo), Zakaria Michael (mwimbaji na mpiga ngoma) na Peter Mashaka (mpiga besi na babatoni). Bendi hiyo sasa ni maarufu kote Afrika Mashariki, ambapo wanaimba mara kwa mara katika maeneo ya umma kama vile vituo vya mabasi, masokoni na kwenye mabaa.
Ben Pol ni mwanamuziki mashuhuri wa Tanzania na mwenye kipaji kinachokua kwa kasi katika anga za muziki za Afrika. Uwezo wake wa kufanya muziki wa mubashara unajumuisha uimbaji kwa sauti ya ubora wa juu na uwezo mzuri wa kutawala jukwaa hivyo kuwa katika kundi la wanamuziki wanaosubiriwa kwa hamu kutumbuiza. Mwimbaji na mtunzi wa nyimbo aliyeshinda tuzo na mwimbaji hodari wa sauti na muziki wa miondoko ya R&B, nyimbo za Ben Pol bado zinaendelea kutamba katika chati mbalimbali za redio. Ametengeneza nyimbo nyingi zilizovuma zaidi, zikiwemo 'Nikikupata', 'Number One Fan', 'Samboira', 'Maneno', 'Moyo Mashine', 'Pete' 'Jikubali', 'Wapo', 'Kidani' na ' Sikukuu'.
Seif Mwinyijuma Haji, maarufu zaidi kama Sholo Mwamba, ni mwanamuziki aliyeshinda tuzo nyingi kutoka Dar es Salaam na mmoja wa waanzilishi wakubwa wa muziki wa singeli Tanzania.
Alihamasishwa kwa mara ya kwanza na marehemu babu yake, ambaye aliwahi kuongoza kikundi cha ngoma ya asili ya Wazaramo. Kwa sasa, wakati akipanua wigo wake wa kutawala jukwaa la dansi barani Afrika, muziki wa singeli wa Tanzania umepiga hatua kubwa kutoka kuonekana kama ‘muziki wa kihuni’ na kuwa fahari ya taifa.
Eneo la wazi la kustaajabisha la jukwaa kuu ndani ya Ngome Kongwe linatoa hamasa kwa wasanii wanaotumbuiza kwenye Sauti za Busara kutoa kilicho bora zaidi. Vivutio vingine katika tamasha lijalo ni pamoja na Siti & The Band kutoka Zanzibar, wanaofanya muziki asilia wa taarab-pop na jumbe zenye mantiki kubwa; Sjava aliyeshinda tuzo, ambaye ni miongoni mwa kundi la wasanii wanaochanganya hiphop na R&B kwa ubunifu na sauti za asili kutoka Kwa Zulu Natal; Suzan Kerunen, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za kisasa kutoka Uganda; Fanie Fayar, mwimbaji na mtunzi wa nyimbo na dansi kutoka Congo Brazzaville ambaye muziki wake unachanganya miondoko ya pop, funk, soul na ala za kitamaduni; Kikundi kinachochipukia cha roots-fusion Zan Ubuntu (Zanzibar) ambacho kimeahidi kutoa burudani ya nguvu jukwaani … na mengine mengi!
Bei maalum zimepangwa kwa Watanzania wote wanaohudhuria tamasha hilo, kwa TSh 6,000/- kwa siku au 16,000/- Tsh kwa pasi ya siku zote 3.
Tamasha la 19 la Sauti za Busara, 11 - 13 Februari 2022 linafadhiliwa na Ubalozi wa Norway, Umoja wa Ulaya, Benki ya CRDB, Zanlink, Emerson Zanzibar na mengine zaidi kuthibitishwa.
Ujumbe kwa wahariri
Pakua picha kubwa za wasanii kwa tamasha la SzB mwaka 2022 hapa: https://www.busaramusic.org/downloads/
This mailing list is announce-only.
Orodha hii ya kutuma barua imekusudiwa tu kueneza habari zinazohusu Tamasha la Sauti za Busara kwa vituo au vyombo vya habari
Sera faragha ya, Busara Promotions Press : Barua pepe zote katika orodha hii itatumika kwa madhumuni ya kukujuza shughuli zote zinazoendelea Busara Promotions. Hazitatolewa wala kupewa mtu mwingine au taasisi yeyote.