Press Kiswahili Message

 
From: "Press Kiswahili" <pressnewsletter_sw@PROTECTED>
Subject: Press Kiswahili Message
Date: February 15th 2022

Taarifa kwa vyombo vya Habari

Februari 14, 2022

Sauti za Busara lahitimishwa huku Serikali ikiahidi kulisaidia tamasha hilo

Zanzibar. Tamasha la 19 lenye hadhi ya kimataifa linalofahamika kwa jina la Sauti za Busara lilifikia kikomo usiku wa Jumapili baada ya burudani ya nguvu ya siku tatu ambalo lilifanyika katika eneo la Ngome Kongwe, Stone Town.

Tamasha la 2022 lilifanyika chini ya Kauli mbiu: ‘Paza Sauti’.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud alibainisha kwamba katika mikono ya watu sahihi, vipaza sauti ni “silaha yetu ya kupambana dhidi ya dhuluma, kujenga amani na umoja duniani kote.”

Pia alisisitiza, “Sauti za Busara si burudani kwa watalii pekee, tukio hili pia ni jukwaa muhimu la kukuza haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na kuheshimu tofauti za kiutamaduni.”

Kwa Zaidi ya siku tatu, vikundi 20 vilitumbuiza kwa msisimko wa hali ya juu watazamaji ambao walikuwa wamesafiri kutoka kote ulimwenguni ili kushuhudia wigo mpana na utajiri wa muziki na vipaji vya Kiafrika.

Kwa watumbuizaji na watazamaji wengi waliohudhuria, huu ulikuwa mtoko wao wa kwanza kwa takriban miaka miwili kutokana na janga la Uviko 19 ambalo lilisababisha kusimama kwa safari za kimataifa na shughuli za kiuchumi.

Wasanii hao walichukuliwa kutoka Mashariki na Kusini mwa Afrika, kwa kuzingatia vizuizi vilivyokuwepo vya kusafiri ambavyo sehemu zingine za ulimwengu bado zinakabiliwa na janga hili.

Kulikuwa na orodha kubwa ya wasanii ambayo ilijumuisha; Siti &amp; The Band, Sholo Mwamba, Vitali Maembe, Ben Pol, Zan Ubuntu, Wamwiduka Band, Nadi Ikhwan Safaa, Upendo Manase na Bahati Female Band wakiwakilisha Tanzania na Suzan Kerunen kutoka Uganda.

Nyota wengine kutoka Kusini mwa Afrika ni pamoja na Sampa The Great kutoka Zambia, Msaki,Sjava na Nomfusi kutoka Afrika Kusini, Evans Pfumela Mapfumo na Sylent Nqo kutoka Zimbabwe, Fanie Fayar kutoka Congo Brazzaville na Aleksand Saya kutoka Reunion.

Akizungumza baada ya onyesho lake Jumapili, Msaki wa Afrika Kusini alisema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwa kwenye tamasha hilo, ingawa alituma maombi mara nyingi ya kushiriki bila ya mafanikio.

Alibainisha Sauti za Busara haikuwa tu ikizungumzia kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika tasnia ya muziki, bali pia kuchukua hatua chanya nyuma ya pazia, kuhakikisha wanawake wanajumuishwa katika majukwaa ya burudani na katika majukumu ya kiufundi.

“Nilifurahia siku mbili nilizoimba hapa, lilikuwa katika tamasha la kufurahisha pamoja na uwepo wa watazamaji wanaojali zaidi wasanii baada ya miaka miwili migumu wakati nchi nyingi zilipokuwa zimefunga mipaka na shughuli mbalimbali,” alisema.

Mwimbaji wa miondoko ya RnB kutoka Tanzania, Ben Pol ambaye pia alikuwa akitumbuiza kwa mara ya kwanza alisema “Nimekutana na watu wengi hapa na kupata marafiki kutoka nchi nyingi duniani wanaojihusisha na muziki wangu.”

Grace Mayala kutoka Dar es Salaam ambaye alihudhuria kwa mara ya kwanza alisema alishawishiwa na marafiki zake ambao wamekuwa wakihudhuria tamasha hilo kwa miakakadhaa.“Sikuwafahamu wasanii wote waliokuwa kwenye orodha ya kutumbuiza awali, lakini muziki wao ulikuwa mzuri hususan burudani ya Sholo Mwamba ambaye alifanya kila mtu acheze,” alisema.

Hata hivyo, siku mbili baada ya Mkurugenzi wa Tamasha hilo kusema hawakuweza kutangaza tarehe za tamasha hilo mwakani kwa sababu ya ukosefu wa fedha, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Mohammed Mchengerwa aliahidi kuunga mkono tamasha hilo.

“Tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha tamasha hili linafanyika tena mwaka ujao,” alisema.

Kwa miaka mingi, tamasha hilo limekuwa likiandaa shughuli mbalimbali ndogo ndogo achilia mbali tukio kuu. Wataalamu wa muziki wa ndani na wageni walijitokeza kwa wingi kushiriki katika onyesho la kila siku la Movers & Shakers meet-and-greet, ambapo lengo kuu likiwa ni lile lile la kukuza sauti za wanawake.

Matukio mengine ni pamoja na Gwaride la Carnival, ushirikiano wa muziki wa Swahili Encounters na majukwaa mengine mawili ya utoaji burudani yalighairishwa kutokana na uhaba wa fedha.

Tamasha la Sauti za Busara la 2022 lilidhaminiwa na Ubalozi wa Norway, Umoja wa Ulaya, Benki ya CRDB, Zanlink, Emerson Zanzibar na wadau wengine.

Taarifa kwa Mhariri

Picha kubwa na muonekano angavu wa Tamasha la Sauti za Busara zinapatikana kwa ajili ya kupakua kupitia https://www.flickr.com/photos/sautizabusara2022/

  • This mailing list is a public mailing list - anyone may join or leave, at any time.
  • This mailing list is announce-only.

Orodha hii ya kutuma barua imekusudiwa tu kueneza habari zinazohusu Tamasha la Sauti za Busara kwa vituo au vyombo vya habari

Privacy Policy:

Sera faragha ya, Busara Promotions Press : Barua pepe zote katika orodha hii itatumika kwa madhumuni ya kukujuza shughuli zote zinazoendelea Busara Promotions. Hazitatolewa wala kupewa mtu mwingine au taasisi yeyote.