Zanzibar: Kwa huzuni na masikitiko makubwa, Busara Promotions inatangaza kusitisha shughuli zake ifikapo tarehe 31 Machi 2022, kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha. Bila fedha za kulipa gharama za ofisi au mishahara, haiwezekani tena kwa taasisi inayosifika kimataifa kuendelea.
Tangu kusajiliwa kwake Zanzibar mnamo Machi 2003, taasisi imekuwa likiutangaza na kusherehekea muziki na urithi wa kitamaduni wa Kiafrika. Kila mwaka mwezi wa Februari, tamasha la Sauti za Busara linalofanyika Mji Mkongwe linavutia maelfu ya wageni kutoka mabara yote kufurahia zaidi ya vikundi 400 vya maonyesho kutoka barani Afrika vikitumbuiza katika majukwaa yake mbalimbali.
Tofauti na mengine, tamasha hili daima liliangazia muziki wa moja kwa moja wenye utambulisho wa kipekee, huku vipaumbele vyake vikiwa kuwapa nafasi wasanii wa kike, wasanii wapya na chipukizi. Iilipinga dhana potofu ya kuwanyima fursa wasanii wasio na majina makubwa, ikajenga umoja na mshikamano hadi nje ya mipaka. Kwa miaka mingi, tamasha limekua nguzo ya mfumo wa ikolojia ya muziki wa Afrika Mashariki, likitoa ajira, kukuza biashara, kutoa mafunzo na kukuza ujuzi, huku likitoa nafasi kwa wasanii ya kujieleza, kushirikiana na mitandao mbalimbali katika tasnia ya muziki.
Wenyeji wengi watakumbuka jinsi tamasha lilivyoubadilisha mwezi wa Februari, kutoka msimu wa chini wa wageni 3,000 waliotembelea Zanzibar mwaka 2004, hadi kufikia wageni zaidi ya 40,000 kwa mwezi huo huo katika miaka ya kabla ya ugojwa wa Uviko -19. Licha ya changamoto za kifedha na zingine tamasha liliendelea, hata wakati wa misimu miwili ya bila umeme kwenye kisiwa chetu, mivutano wa kisiasa na janga la ulimwengu la corona.
Haya yote yasingewezekana bila msaada wa wahisani, wafadhili na washirika, hasa Ubalozi wa Norway jijini Dar es Salaam, ambao ulitoa ufadhili wa kuendesha shirika ili kuendeleza na kutekeleza mipango mkakati wake wa kuanzia Oktoba 2009 hadi Machi 2022.
Usaidizi wa kifedha wa Norway umefikia mwisho wake mwaka huu. Kwa bahati mbaya, bila ufadhili mwingine wa sekta ya umma au binafsi, Busara Promotions haiwezi kuendelea kuwepo.
Uongozi na Bodi inachukua fursa hii kuwashukuru wasanii na watazamaji wote, wafanyakazi wahisani, wafadhili, vyombo vya habari na washirika wengine kwa msaada wao kwa kipindi chote. Yusuf Mahmoud, mwanzilishi na mkurugenzi "namshukuru Mwenyezimungu kwa kufanikisha tamasha kwa miaka yote hii 19, timu yetu inajivunia mafanikio yake na tunaomba urithi wetu uendelee na udumu kwa muda mrefu." Asanteni.