PRESS RELEASE
for publication 21 Nov 2022
Sauti za Busara yazindua orodha ya nguvu ya wasanii kusheherekea miaka 20
Zanzibar. Waandaji wa Tamasha maarufu la muziki wa Kiafrika la Sauti za Busara ambalo hufanyika Mji Mkongwe, Zanzibar kila Februari, wametangaza orodha ya wasanii itakayolifanya toleo la ishirini la mwaka wa 2023 liwe la kukumbukwa.
Likishirikisha bendi maarufu na zinazochipukia kutoka kanda zote za Bara la Afrika, likiongozwa na msanii nguli wa muziki wa reggae barani Afrika Tiken Jah Fakoly, kutoka Ivory Coast, Kwa lugha ya Kifaransa, Kiingereza, Dioula na Bambara, maneno yake yanazungumzia ukosefu wa haki wanaotendewa Waafrika. Wito wake ni umoja wa Afrika na kufufuka kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Akiwa na zaidi ya albamu kumi na mbili maarufu zilizotolewa tangu 1996, Tiken Jah Fakoly mara kwa mara hujaza viwanja vya soka anapotumbuiza kote barani Afrika, Ulaya na kwingineko.
BCUC, kutoka Soweto Afrika Kusini, hucheza muziki ‘kwa ajili ya watu na watu pamoja na watu.’ BCUC walivutia sana tamasha la Sauti za Busara la mwaka 2019, ambapo jumbe zao za nguvu na onyesho lao vilisifiwa sana na wote waliohudhuria. "Tunajiona kama wapigania uhuru wa kisasa ambao wanapaswa kuelezea ulimwengu hadithi ya zamani, ya sasa na ya baadaye kuhusu Soweto," anasema 'Jovi' Nkosi, mwimbaji mkuu.
Mwakilishi wa singeli mwaka huu atakuwa Mzee wa Bwax, ambaye pia anaahidi onyesho ambalo watu hawatalisahau. Wasanii wengine wa Tanzania watakaoshirikishwa ni pamoja na Patricia Hilary, Damian Soul, Zawose Reunion, Stone Town Rockerz, Uwaridi Female Band, Zan Ubuntu, Supa Kalulu, Zenji Boy na Wenzake, Waungwana Band and Culture Musical Club, taarab asilia ya Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 1958.
Wasanii wengine wa kimataifa Februari ijayo ni pamoja na Asia Madani, msanii mwimbaji kutoka Sudan ambaye muziki wake unaonyesha kujivunia urithi wake kama mwanamke shupavu wa Kiafrika kupitia sauti yake murua. Naxx Bitota kutoka DRC huchanganya rumba ya Kongo na mutuashi na mitindo mingine ya muziki na reggae, rumba na afropop. Sana Cissokho ni msanii maarufu wa kora kutoka Senegal, anaeendeleza urithi wa kitamaduni wa Mandinka. Atse Tewodros Project mchanganyiko wa wanamuziki wa kitamaduni wa Ethiopia na Italia. Muziki wao unajumuisha nyimbo za mapambano ya Waethiopia dhidi ya Waitaliano. Kama ilivyoelezwa na kiongozi wao wa bendi Gabrielle Ghermandi, "Muziki hupaza sauti kubwa kwa sauti zilizojificha. Muziki ni njia ya kutoa maono ya wakati ujao unaowezekana au usiowezekana."
Sauti za Busara 2023 pia inaahidi maonyesho bora kutoka kwa Majestad Negra, kikundi cha dansi kutoka Puerto Rico, Kaloubadya, kikundi cha maloya kutoka Reunion, Nasibo, mwimbaji- mtunzi- mtumia zana ya mbira kutoka Zimbabwe, na Zily, mwanamke mwingine shupavu ambaye muziki wake umejikita kwenye mila za utamaduni wa Mayotte.
Kaulimbiu ya tamasha lalijalo ni Tofauti Zetu, Utajiri Wetu: Our Wealth is in Our Diversity. Kama mkurugenzi wa tamasha Yusuf Mahmoud anavyoeleza, ‘Tamasha linaangazia ubora na muziki wa aina mbalimbali kutoka kote barani Afrika, hasa wanamuziki wa kike, chipukizi wenye sauti za kipekee, jumbe zenye nguvu, msisimko na wanaovutia jukwaani. Wanaotembelea tovuti yetu wanaweza kutazama video na kujua zaidi kuhusu vikundi vyote vitakavyotumbuiza Februari ijayo katika toleo hili maalum la maadhimisho ya miaka 20.’
Kulikuwa na maswali mengi baada ya miaka mingi ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway kuisha Machi 2022, kisha kuvunjika kwa mkataba wa Blue Amber Resort miezi sita baada ya kusaini makubaliano, Busara Promotions, taasisi inayoandaa tamasha, likikaribia kufunga milango yake. Kama ilivyotangazwa mwezi mmoja uliopita, Fumba Town, mradi wa CPS iliokoa jahazi kwa kuingia makubaliano ya kulipia gharama uendeshaji wa taasisi ya Busara Promotions hadi Machi 2025. Tobias Dietzold, Afisa mkuu wa biashara alisema wakati wa kusaini makubaliano, "Tumejitolea kufanya tamasha la Sauti za Busara liwe imara na kwa miaka michache ijayo huku tukifurahia utajiri na urithi wa tamaduni zetu mbalimbali kupitia muziki. Kupitia ushirikiano huu, tutahakikisha kwamba tunatoa mchango wetu mdogo, kwa miaka mitatu ijayo ili kuhakikisha tamasha linaendelea kuwepo kwa ustawi wa tamaduni,”
Sauti za Busara linajulikana na BBC, CNN, OkayAfrica, Afropop Worldwide na wengineo kama ‘moja ya matamasha bora ya muziki na yanayoheshimika zaidi barani Afrika’. Toleo la 20 litafanyika Mji Mkongwe, Zanzibar kuanzia tarehe 10 – 12 Februari 2023 huku kiingilio kwa Watanzania zikigharimu shilingi 20,000/- tu (siku tatu), au 10,000/- kwa tiketi ya siku moja.
Sauti za Busara 2023 inawezeshwa na Fumba Town, a project by CPS; Ignite Culture, Kendwa Rocks, Zanlink, Institut Français, Australian High Commission, Emerson Zanzibar and more to be confirmed.
Kwa maelezo zaidi :www.busaramusic.org
\\ENDS\\
Note to Editors:
Download Sauti za Busara hi-res photos and more at www.busaramusic.org/downloads