Mpendwa Familia ya Busara ,
Kwanza kabisa, tunapenda kuwatakia Mwaka Mpya mwema uliojaa afya njema, mafanikio na baraka tele!
Tunafuraha kufungua nanyi ukurasa mpya muhimu katika safari ya tamasha la Sauti za Busara. Kutokana na kazi kubwa za ukarabati zinazoendelea katika eneo la kihistoria la Ngome Kongwe, toleo la 23 la Tamasha Rafiki Zaidi Duniani litahamia katika eneo jipya la wazi — Viwanja vya Mnazi Mmoja, Mji Mkongwe, Zanzibar.
Baada ya miaka 22 ya kipekee ya kufanyika kwa tamasha letu ndani ya Ngome Kongwe, mabadiliko haya yanatufungulia fursa mpya na za kusisimua. Eneo jipya limezungukwa na miti mizuri, lina nafasi pana, na hupata upepo mwanana wa baharini — likiwa na mazingira bora zaidi kwa muziki, burudani, masoko, chakula, na nyakati za kukumbukwa za kushirikiana. Pia linatuwezesha kupokea idadi inayoongezeka ya mashabiki kwa faraja zaidi, huku ttukiweka kumbukumbu mpya kwa wapenda tamasha na wasanii wetu.
Dhima ya Sauti za Busara inabaki kuwa ie ile — muziki wa Afrika, umoja na mshikamano, sasa tukiwa na nafasi kubwa zaidi ya kukua na kusherehekea.
Karibu uwe pamoja nasi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kwenye toleo linalotarajiwa kuwa la kusisimua zaidi kuwahi kutokea!
Kwa heshima na shukrani,
Timu ya Busara Promotions