Mama C And The Fusion Band
Mama C and The Fusion Band ni bendi yenye nguvu kutoka Arusha, Tanzania, inalojulikana kwa kuchanganya sauti za asili za Kiafrika na mitindo ya kisasa, na kutengeneza muziki wenye mizizi ya kitamaduni unaogusa hadhira ya kimataifa. Kundi hili lilianzishwa na kuongozwa na Charlotte Hill O’Neal, anayefahamika sana kama Mama C au Iya Osotunde Fasuyi, na linaakisi dhamira yake ya maisha ya kutumia sanaa, harakati na kuhamasisha jamii.
Mama C alizaliwa Kansas City, Kansas (Marekani) na alijiunga na Black Panther Party akiwa na umri wa miaka 18. Yeye na mumewe Pete O’Neal walihamia Tanzania mwaka 1972, kama sehemu ya harakati ya Pan-Africanism duniani. Mwaka 1991, waliasisi kituo cha United African Alliance Community Center (UAACC) katika kijiji cha Imbaseni, nje kidogo ya Arusha, taasisi ya kijamii inayotoa mafunzo ya bure ya sanaa, elimu, na stadi za kazi kwa vijana wa eneo hilo. Urithi huu wa kazi ya jamii umejikita sana katika ujumbe na dhamira ya Mama C and The Fusion Band.
Muziki wao ni mchanganyiko wa urithi wa Kiafrika na ubunifu wa kisasa, ukihusisha ala mbalimbali kutoka kila pembe ya bara la Afrika, kama vile Kamalen ngoni (Afrika Magharibi), Nyatiti na Obokano (Kenya), Zeze na Kalimba (Afrika Mashariki na Kusini), Berimbau (Afro-Brazilian), pamoja na ala za kitamaduni za ngoma, gitaa, kinanda, drum kit, na ala zingine za umeme.
Muziki wao umejaa tungo za kuvutia, ushairi (spoken words), na muziki wa kufoka foka (hip-hop), ukiangazia mada nyeti na muhimu kama Haki za kijamii na ukombozi, Usawa wa kijinsia, Utambulisho wa kitamaduni na Fahari yake, Uelewa wa mazingira, Mazungumzo kati ya vizazi na tamaduni tofauti.
Ingawa wamejikita kwenye ardhi ya Tanzania, sauti yao imevuka mipaka. Wametumbuiza katika vijiji vya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, mikutano ya kimataifa, na makongamano ya wanadiaspora barani Afrika, Ulaya, na Marekani. Iwe jukwaani au darasani, Mama C and The Fusion Band hutoa maonesho yaliyojaa ujumbe, ubunifu, na utu wa kweli.

