Man Fongo
Man Fongo ni jina linalojulikana sana katika tasnia ya muziki wa Singeli, na anachukuliwa kuwa mmoja wa waanzilishi wa mtindo huo nchini Tanzania.
Amezaliwa na kukulia Dar es Salaam, na alianza safari yake ya muziki mwaka 2006 kama DJ wa mtaani, akipiga muziki wa kienyeji uliojulikana kama Vigodoro. Muziki wa vigodoro ulipendwa sana kwenye mitaa ya Dar es Salaam na ulijulikana kwa kuvutia watu wengi kwa sherehe za usiku kucha.
Mwaka 2010, Man Fongo aliamua kuingia rasmi kwenye muziki wa Singeli kama mwimbaji. Alitoa wimbo wake wa kwanza uitwao "Simuamini Mganga", ukifuatiwa na nyimbo nyingine kama "Police Babylon", na nyinginezo.
Kipindi chake cha mafanikio makubwa kilikuja mwaka 2016 baada ya kuachia wimbo maarufu "Hainaga Ushemeji", uliompa umaarufu mkubwa na kumweka kwenye ramani kama mmoja wa wasanii bora wa Singeli nchini Tanzania.
Man Fongo amewahi kutumbuiza katika majukwaa ya ndani na ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Singeli Fest (Tanzania), Boiler Room (Tanzania), na Indian Ocean Music Market (Reunion Island).

